Tuesday, June 19, 2012


Mwanafunzi akilia na Katiba

Johnseverini Mkini
KATIBA ni Sheria Mama ambayo ni mkataba kati ya Mtawala (serkali ) na Raia. Kwa maana halisi ni kwamba, Katiba ni mali ya Raia wa Tanzania ambayo inatoa ufafanuzi kwa Mtawala jinsi ya kufuata taratibu za kumtawala Raia mwenye katiba.

Kwa maana hiyo, Katiba ni mali ya Watanzania wote, na siyo mali ya SERKALI., hivyo basi Serkali inatumia Katiba kuongoza nchi na watu wake bila kwenda kinyume kwa mujibu wa taratibu na, Katiba itumiwe na raia wote bila kuangalia Ukabila, dini, rangi au madaraka.

(ii) Kwa kuwa Katiba ni Sheria Mama, asiweko mtu, au raia kuwa juu ya KATIBA, bali watu wote bila kujali madaraka, watakuwa chini ya Katiba.

(iii) Katiba ni sheria mama ya nchi kwa raia wote, hivyo kwenye katiba mpya, kiondolewe kipengele cha kumkinga Rais kutoshitakiwa pindi anapothibitika kuwa ametenda makosa ya kuvunja katiba anapokuwa madarakani, kwa manufaa binafsi au familia yake, jamaa au rafiki.

Mbali na kushtakiwa kiongozi husika aondolelwe/asimamishwe uongozi mara moja (Impeachment) kwa manufaa ya umma kwa kufuata taratibu.

Mgawanyo wa madaraka ya viongozi kikatiba
Mmiliki wa Katiba:- Kimsingi, Katiba ni mali ya raia wote wa nchi ya Tanzania. (Serkali itaitumia Katiba kama ni moja ya vitendea kazi vyake tu) ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa kila raia anafuata sheria na taratibu za nchi,na kila raia anapata haki zake zote za msingi anazostahili, (kwa kifupi, Serkali ni msimamizi mkuu wa kuhakikisha kuwa Katiba inatumika kama ilivyokusudiwa na raia wake wote).

Mahakama:
Mahakama ni chombo (Mhimili huru). Muhimu ambao una majukumu ya kutafsiri sheria zote za nchi zitokanazo na Katiba na zile zinzotungwa Bungeni baada ya kuzingatia Katiba.

Pendekezo:- Mahakama uwe mhimili huru usiofungamana na Serkali ili uweze kutenda haki katika kazi zake za kila siku.
Majaji wa mhimili huo, wasiwe wateule wa Rais, (wachaguliwe na Bunge )na mahakimu wa mikoa na wilaya na mahakama za mwanzo wote wawe waajiriwa wa Mahakama Kuu.

Madaraka ya Rais
Kumekuwapo na utendaji mbovu na usioridhisha wa watumishi wa Serkali wanaoteuliwa na Rais ambaye pia ni mkuu wa nchi, ambapo baadhi ya nyanja muhimu hazileti matokeo mazuri kwenye miradi ya maendeleo ambayo inatengewa fedha na Bunge kama ilivyokusudiwa, kwa kukosa wasimamizi mahiri ambao wengi wao ama wanateuliwa kwa kufahamiana, au kwa urafiki, au kwa kulipwa fadhila lakini hawana uwezo kiutendaji.
Kwa hiyo iko haja ya kupunguza madaraka aliyopewa Rais ya kuteua watendaji kadhaa wa ngazi mbali mbali kitaifa ambao hawana tija kwa jamii, zaidi ya kukilinda chama cha siasa kinachokuwepo madarakani kwa wakati husika.
Kwa mfano:- Uteuzi wa Mkuu wa mkoa (RC) sanjari na RAO kwa ngazi ya mkoa, na DC na DAO kwa ngazi ya wilaya, vyeo ambavyo vilibuniwa na Wakoloni, vikiwa ni daraja la utawala kulinda maslahi ya Gavana kutoka Mikoani na Wilayani. Kwa sasa hivi hatuna wakoloni, hivyo sababu ya kuwa na vyeo hivyo haipo tena, kwa kuwa vyeo hivyo havina tija kabisa kwa walipa kodi na ni ufujaji wa fedha za serkali.
Permanent Secretaries (Makatibu wakuu wa wizara) na wakuu wote wa mashirika ya umma,wote hao ni wateule wa Rais kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakionekana kisiasa zaidi kuliko kuwa watendaji wa serkali kwenye maeneo yao ya kazi na,mara nyingine wakingilia kazi za mtendaji wa Halmashauri za Wilaya na za Miji.
Lakini, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ni mtu anayewasiliana moja kwa moja na raia vijijini, na mijini katika shughuli zote za maendeleo za kila siku. Hata matumizi mabaya ya fedha za miradi husika, anayekaguliwa mahesabu na kuadhibiwa pindi anapobainika kuwa na makosa, ni Mkurugenzi wa Halmashauri, wakati DC na Mkuu wa Mkoa wakiwa nyuma ya pazia hawaonekani, wala hawaguswi. Huo ni uonevu kisiasa.

Pendekezo (a)
Kwa maana hiyo, hakuna haja ya kuwapo vyeo vya, RC, RAO, DC, na DAO kwa hiyo ingefaa vifutwe kama vilivyofutwa vyeo vya RDD na DDD na kubakiza cheo cha DED na watendaji wake wote katika ngazi ya wilaya, ambao Katiba itamke kuwa hao waajiriwe kulingana na taaluma zao. Lakini uwepo utaratibu wa kiutawala wenye kuunganisha madaraka katika nyanja za ulinzi na usalama kazi ambazo zitafanywa na Disrict Executive Director baada ya cheo cha DC kuondolewa.
Pia Taasisi Kupambana na Kuzuia Rushwa, DPP(Mkurugenzi wa Mashtaka) na DIC (Mkurugenzi wa Upelelezi, na Mwanasheria Mkuu wa Serkali (A.G) hawa wameonyesha udhaifu mkubwa sana katika kufanya kazi zao kwa haki hasa inapodhihirika, kuwa Mtuhumiwa anayepaswa kukamatwa, kupelelezwa na kushtakiwa na kuhukumiwa, anatoka sehemu nyeti, au ni mteule wa Rais basi utaona hapo haki ikipindishwa ili kumwokoa mhusika.

Pendekezo (b)
Vyeo hivyo vya TAKUKURU, DPP, DIC na AG viwepo lakini visitokane na uteule wa Rais, ili waweze kufanya kazi yao bila upendeleo, lakini wawe Watanzania wenye taaluma husika na uwezo wa kufanya kazi hizo, waombe kazi na kusailiwa na Bunge, kisha Rais atawaapisha, lakini wote hao watawajibika bungeni.Source: Mwananchi 18/06/2012

No comments:

Post a Comment